Nyota wa muziki wa bongo flava nchini Diamond Platinumz amewataka
wasanii wa Tanzania kusambaza nyimbo zao kwa njia ya teknolojia kama
vile Mziiki iliyozinduliwa hivi karibuni ili ziweze kuwafikia watu wengi
na kwa wakati huohuo wanamuziki pia kunufaika na jasho lao.

Diamond anasema kuwa ameamua kazi zake kuziingiza sokoni tofauti
na kazi zake za nyuma ambapo baada ya kushauriana na wadau
anaoshirikiana nao kikazi ameamua aingie sokoni kwa njia ya kidigitali
kupitia programu ya Mziiki iliyozinduliwa hivi karibuni ambayo pia yeye
ni balozi anayeitangaza.
Anasema Tanzania ina wanamuziki wengi wenye vipaji lakini wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiwafanya wasifike
mbali zaidi ya muziki wao kusikika hapa nchini na wengi wao kutamba kwa
muda mfupi na kupotea katika ulimwengu wa muziki huku wakiwa
hawajanufaika na kitu chochote kimaisha na kushauri kuwa wasibaki nyuma
kiteknolojia hasa wakati wa kupeleka kazi zao sokoni iwapo watataka
kujikwamua.
“Licha ya kuwepo na changamoto kubwa kama vile kutokuwepo sheria ya
hakimiliki inayopelekea wasanii kuibiwa kazi zao na kazi za muziki
kutumiwa na vyombo vya habari kama redio na televisheni bila kuwalipa
wahusika chochote. Tatizo lingine linalodumaza muziki wa Tanzania ni
uoga wa wanamuziki kubadilika na kuogopa teknolojia za kisasa kama hii
programu ya kupakua muziki kwenye simu kwa kupitia Mziiki” Alisema.
Amesema sababu kubwa iliyopelekea kuamua kufanya biashara ya
muziki kupitia progamu hii ni kwamba nyimbo zake ziweze kuwafikia
washabiki wake popote na muda wowote kwa urahisi kupitia simu zao za
mkononi na anakuwa na uhakika wa kupata mapato tofauti na kama
zinavyosambazwa na wasambazaji wa mtaani.
“Duniani kwa sasa hivi kuna ushindani mkali katika nyanja zote.
Sisi kama wanamuziki wa Tanzania tunapaswa kuhakikisha tunatoa muziki wa
viwango vya juu na kuhakikisha tunalenga zaidi katika masoko ndani na
ya nje kama wenzetu wanavyofanya kusambaza kazi zao kupitia kampuni
zinazotumia teknolojia ya kisasa na kumnufaisha msanii kama ilivyo
program hii ya Mziiki. Kuna umuhimu mkubwa wa kujiamini, kufanya vizuri
ili tuweze kutangaza Tanzania, kutangaza lugha ya Kiswahili na kupata
mapato ya kutosha kutokana na kazi ya muziki ambayo ikifanywa kitaalamu
inalipa kwa kiasi kikubwa” anasema Diamond Platinumz
Aliwaomba wapenzi wa muziki nchini kuwaunga mkono wanamuziki wa
hapa nchini kwa kupakua nyimbo zao kwenye Mziiki kwa kuwa njia hii iko
wazi na inamuwezesha mwanamuziki kujua kirahisi jinsi kazi zake
zinavyokubalika sokoni na inamuwezesha kujua mapato yake tofauti na njia
nyingine kama uuzaji wa CD kwenye maduka na mitaani.
Programu ya Mziiki ambayo ilizinduliwa na Vodacom kwa kushirikiana
na Spice VAS Africa imeanza kufanya kazi na wanamuziki wa hapa nchini
na nje ya nchi na katika kipindi cha muda mfupi tayari imesajili
wanamuziki wapatao 1,000 ambao kazi zao hususani zile mpya
zitasambazwa kwa njia ya kidigitali na malengo yake makubwa ni
kuhakikisha wanamuziki wanapeleka kazi zao sokoni kwa haraka na
kunufaika na jasho lao hususan pale ambapo wananchi wengi watatumia
mtandao kwenye simu zao kupakua nyimbo wazipendazo za wanamuziki ambao
wamejiunga kwenye tovuti ya kampuni hiyo ambayo inapatikana kwa kubofya
tovuti ya www.mziiki.com.
No comments:
Post a Comment