KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mamia ya wanafunzi wa Kitanzania
wanaosoma katika shule za msingi nchini Kenya, wameripotiwa kufukuzwa
nchini humo.
Tayari 50 kati yao, wamerejeshwa nchini huku wengine kadhaa wakiwa bado
wamekwama katika eneo la Narok Magharibi. Baadhi ya walioathirika ni
wale ambao wako katika hatua za mwisho za kuhitimisha elimu yao ya
msingi katika darasa la nane.
Vijana hao wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kumaliza shule Oktoba
mwaka huu ; na kufukuzwa kwao kunawaweka katika wakati mgumu zaidi
kimasomo.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mgandilwa alikiri kuwepo na tatizo
hilo na alilieleza gazeti hili jana kuwa: “Ni kweli wanafunzi wetu
waliokuwa wanasoma Kenya wamefukuzwa nchini humo na 44 kati yao
wamesharudi nchini, ila tuna wasiwasi kwamba mamia wengine watakuwa bado
wamekwama huko na tuko mbioni kuwafuatilia zaidi.”
Meneja wa Baraza la Wafugaji katika Tarafa ya Ngorongoro, Peter Metele
naye alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuongeza kuwa yeye ndiye
anayefanya kazi ya kwenda kuwachukua wanafunzi waliotimuliwa Kenya.
Imeelezwa kuwa chanzo cha kutimuliwa kwa watoto hao ni msuguano,
ulioibuka baada ya kufanyika kwa operesheni maalumu ya kuwaondoa
wahamiaji haramu kutoka nchi jirani ya Kenya, wanaodaiwa kuvamia maeneo
ya Loliondo na Sale.
Hadi sasa watoto 27 wamehifadhiwa kwenye nyumba ya kulala wageni ya
Cobra katika eneo la Wasso, Loliondo. Wengine takribani 10 wamepelekwa
kwenye kata ya Arash na waliobakia wako majumbani mwao.
“Tumewahifadhi kwenye nyumba za kulala wageni kwa sababu kuna wale
wanaotoka vijiji vya mbali sana na tunataka tujitahidi kufanya
mazungumzo na viongozi wa upande wa Kenya ili waruhusiwe kurejea
mashuleni, iwapo tutafanikiwa basi iwe rahisi kuwarudisha Kenya,”
alisema Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro, Metili.
Imedaiwa kuwa wanafunzi waliofanikiwa kurejeshwa ni wale wanaodhaminiwa
na Baraza la Wafugaji na wale waliopelekwa na taasisi mbalimbali, ambao
ilikuwa rahisi kutumiwa usafiri, ila kwa waliopelekwa na wazazi wao,
bado wamekwama Kenya.
“Tulishafanya mazungumzo ya awali na viongozi wa upande wa Kenya siku ya
tarehe 12 Mei mwaka huu, lakini ingawa tulikubaliana mengi, ikiwemo
wafanyabiashara wetu kuruhusiwa kupeleka bidhaa Kenya inaonekana kuwa
wananchi wa Narok wao wana maamuzi yao tofauti na serikali yao hivyo
wanasisitiza kuendeleza mzozo, na sasa wameamua kuongeza tatizo kwa
kuwatimua watoto,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Wafugaji, Ngorongoro, James ole
Moringe alisema baraza hilo pia linafanya jitihada za kukutana na
viongozi wa Narok na walimu wa huko ili kupata mwafaka wa suala hilo.
Akisimulia, mmoja wa wanafunzi hao, Lilian Peter (14) anayesoma darasa la Nane katika
Shule ya Ilkerin-Loita, alisema Chifu wa eneo hilo alifika shuleni kwao
na kuwaita walimu ofisini, kisha baadaye Mwalimu Mkuu, Abel Githinji
alianza kuingia madarasani na kuwatoa wanafunzi wote wa Kitanzania huku
akiwaagiza wafungashe virago.
Wengi wa wanafunzi hao ni wale wanaotoka kwenye tarafa mbalimbali za
wilaya ya Ngorongoro, ambayo imepakana moja kwa moja na Kaunti au Jimbo
la Narok, Kenya.
Mwanafunzi mwingine, Naini Petey ambaye anasema wenzao wanaosoma shule
nyingine ya Naikara, pia walifukuzwa na wengi wao bado wamekwama nchini
Kenya, wakisubiri wazazi au wafadhili waende kuwachukua.
Juhudi za gazeti hili kuwapata mawaziri wenye dhamana ya mahusiano ya
kimataifa, Bernard Membe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa na Dk Harrison Mwakyembe wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, hawakupatikana katika ofisi zao, kwa njia za simu na hata
bungeni Dodoma kuweza kuzungumzia suala hilo.
Chanzo: Habari Leo

No comments:
Post a Comment