![]() |
| Tundu Lissu |
Ni kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere, maana Mwalimu pamoja na waandishi habari Robert Makange (mhariri wa gazeti la Sauti ya TANU) na Rashid Baghdelleh (mhariri wa gazeti la Mwafrika) walikuwa watu wa kwanza Tanganyika kushtakiwa, na kupatikana na hatia, kwa kosa la uchochezi.
Sheria iliyotumika wakati huo ni hii hii inayotumika dhidi yetu, miaka 58 baadae. Tofauti pekee ni kwamba wameihamisha kutoka kwenye Kanuni ya Adhabu na kuipeleka kwenye Sheria ya Magazeti.
Na kama ambavyo kuitwa mchochezi na kushtakiwa kwa Mwalimu Nyerere hakukuwa taji la miba kwake, hivyo hivyo kushtakiwa kwetu kwa makosa hayo hayo hakutakuwa taji la miba kwetu.
Sisi ni wajukuu wa Julius Kambarage Nyerere na Robert Makange na Rashid Baghdelleh. Hii ni heshima kubwa kwetu, sio jambo la kuinamisha kichwa kwa aibu. William Rivers Pitt, mwandishi wa Kimarekani aliandika kitabu kìitwacho 'Silence is the Greatest Sedition', yaani 'Ukimya ndio Uchochezi Mkubwa.'
Ukimya wakati katiba na sheria na haki zetu zinakanyagwa na Mtakatifu Rais na watu wake ndio uchochezi mkubwa. Sisi hatujafanya kosa hilo. Kwa sababu hiyo, tunawasubiri watesi wetu wa sasa mahakamani waje watuambie makosa yetu ni yapi. Na tayari wameshaanza kukimbia, maana aliyetushtaki sisi hataki kuja kutoa ushahidi mahakamani. Watakimbia sana. Aluta continua!
