| Nahodha wa Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' |
Mchezaji huyo mwenye heshima kubwa ndani ya Yanga, ametumia siku tatu kupambana juu chini kwenye kambi ya Taifa Stars kumshawishi straika wa Mgambo, Malimi Busungu aachane na Simba na kutua Yanga.
Simba ilifanya mazungumzo na kukubaliana na mchezaji huyo na ilitegemea kwamba ni mmoja wa wachezaji watakaofufua matumaini yao msimu ujao, lakini ghafla upepo ukabadilika na wakashika mdomo kusikia Yanga imemnasa na kumsajili.
Cannavaro alikuwa akimjaza upepo Busungu akisaidiwa na Salum Telela ambapo pia walikuwa wakiipiga presha Kamati ya Usajili imsajili mchezaji huyo haraka ili asije akaenda Simba.
Wachezaji hao wanaocheza nafasi ya ulinzi walisimamia shoo hiyo kutokana na jinsi mchezaji huyo alivyokuwa akijituma mazoezini pamoja na kuwatoa jasho, huku watu wa Simba wakimfuatilia kwa karibu sana na kupata sifa zake kwa Kocha wa Stars, Mart Nooij kwamba ni jembe.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba wachezaji hao waliiambia kamati ya usajili ya Yanga chini ya Mhandisi Isaac Chanji kwamba Busungu asiposajiliwa wasilaumiane msimu ujao.
“Hatukujua walitumia ushawishi gani mpaka wakampa akili ya mchezaji mwenyewe kukubali kirahisi kuja kusaini, walitumbia wazi tusifanye kosa Busungu akatua Simba tutalia,”alidokeza kigogo mmoja wa kamati ya usajili Yanga.
Busungu alithibitisha ushawishi huo uliofanywa na Cannavaro akisema alifanya kazi kubwa kurahisisha azikatae Sh30 milioni za Simba. “Unajua unapofika usajili kama hivi si kwamba kila mchezaji atapenda usajiliwe, lakini nasema wazi kwamba Cannavaro na wenzake ni kweli walitumia siku tatu kunishawishi,”alisema Busungu.
Busungu amekabidhiwa jezi namba 16 atakayoitumia ndani ya miaka miwili ya mkataba wake. Hiyo inathibitisha kufunguliwa milango ya kiungo Nizar Khalfan ambaye Mwanaspoti liliandika mapema kwamba hataendelea Jangwani.
No comments:
Post a Comment