Pages

Sunday, 7 June 2015

Kocha Yanga asajili kiboko ya Msuva

Simon Msuva
KOCHA wa Yanga, Hans Pluijm, anaishi Ghana na familia yake. Kwenye Jiji la Accra anakoishi mvua imeleta shida na sasa ni mafuriko na majanga kila kona sambamba na miji mingine ya Ghana.
Mvua zimekuwa kero kubwa kama ilivyokuwa katika siku za hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Accra hadi usafiri umekuwa ni tatizo kubwa ambako watu wanalazimika kutembea kwa miguu kwa vile magari hazitembei kutokana na madaraja kuvunjika, barabara kuharibika pamoja na foleni. Hali hiyo imemboa Pluijm lakini amemaliza likizo yake na kesho Jumapili usiku atatua Dar es Salaam kuanza kibarua cha kuisuka Yanga.
Jana Ijumaa alipiga stori mbili tatu na Mwanaspoti akitaka kujua hali inavyoendelea nchini lakini akadokeza jambo moja linalohusu usajili wa Yanga.
Kocha huyo alisema kwamba nguvu zake sasa ameelekeza kwa wachezaji watatu tu na kati yao anataka wawili wawe kiboko ya Simon Msuva na Juma Abdul.
“Ukiangalia Msuva (Simon) anaweza kuondoka wakati wowote, ni lazima tujiandae kwa kupata mtu kama yeye au zaidi lakini pia nataka beki wa kulia mwenye makali zaidi ya Juma (Abdul) kuongeza ushindani hapo tunaweza kusema kidogo tumekamilisha timu yetu,”alisema Pluijm.
“Najua kila kitu kinachoendelea huko, nafurahi kuona kuna kazi nzuri imefanyika waliosajiliwa naamini watatusaidia lakini bado tunahitaji watu hao zaidi.”
Pluijm amemtaja mshambuliaji Donald Ngoma wa Zimbabwe kama mmoja wao ingawa Wabongo hakuwataja.
Mholanzi huyo alisema mbali na Ngoma ambaye usajili wake akitoka FC Platinum umezuiwa kwa muda wakisubiri maamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya idadi ya wachezaji wa kigeni, pia anataka apatikane kiungo wa pembeni mmoja hasa kulia huku pia akitaka beki wa kulia atakayesaidiana na Juma Abdul.
Alisema pia anataka kuja kuangalia uwezo wa kiungo raia wa Sierra Leone Lansana Kamara ambaye amemtaka kusubiri jibu lake kwa siku chache baada ya kuanza majaribio. Lakini habari za ndani ya Yanga zinadai kwamba Kamara amewaambia viongozi kwamba yeye amekamilika na si mtu wa kujaribiwa.

No comments:

Post a Comment