Pages

Tuesday, 16 June 2015

NI ZAMU YETU KUWAHOJI WAGOMBEA

Mwenyekiti wa tume ya katiba, Jaji Damian Lubuva.
Wote tulio hai tena wenye afya tele hatuna budi kumtukuza Mungu muumba wa mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Baada ya kusema hayo niwakumbushe tu kwamba kila unapofanyika uchaguzi mkuu wa nchi, wabunge wengi hawarudi bungeni, yaani wanatemwa na wapiga kura wao  kwa maana ya kushindwa kwa kura katika uchaguzi huo, ama kutopitishwa na vyama vyao kugombea tena nafasi hiyo.

Hivi sasa kila kona ya nchi, joto la uchaguzi limepanda na baadhi ya wabunge sasa wanakacha bunge wanajikita kwenye majimbo yao kwa nia ya kuweka mambo sawa, yaani wanajipitishapitisha.
Ukweli ni kwamba imebaki miezi takriban minne ufanyike uchaguzi huo. Hiki ndicho kipindi ambacho wananchi katika majimbo humwagiwa zawadi za kila aina, wapo ambao watapewa au wanapewa kofia ‘kapelo’, fulana, kanga na hata kupewa fedha na wagombea  ili wawapigie kura siku ya kupiga kura.
Achilia mbali zawadi hizo, zipo ahadi nyingi zilizotolewa mwaka 2010 na wabunge wakati wakiomba kura, lakini hazijatekelezwa. Wanachotakiwa kukumbuka wananchi kabla ya kupokea zawadi za waheshimiwa mwaka huu ni kujikumbusha ahadi zao na kuwauliza zile ambazo hawajazitekeleza za mwaka 2010.
Yale mazoea ya kijinga kwamba kila unapofikia  uchaguzi kuwa ni kipindi cha kudanganywa, kuahidiwa na mengineyo mengi ilimradi wahusika waweze kutimiza azma yao ya kuukwaa ubunge, mwaka huu tusikubali hasa kama mhusika hakuna alichofanya kwa miaka mitano aliyotutumikia.
Ahadi zinazotolewa kipindi kama hiki huwa tamu, lakini tatizo kubwa huwa katika utekelezaji na baadhi ya wagombea wakishapata uongozi hubaini kuwa waliahidi mambo makubwa kupita uwezo wao. Kwa bahati mbaya wakati wakibaini hilo wanakuwa kwenye wakati mgumu wa kusema ukweli ndiyo maana nasisitiza kuwa ni lazima tuwahoji maswali watakapokuwa mbele yetu.
Kungekuwa na sheria kabisa ya kuwabana wasema uongo kwa hawa wanaokuja mbele yetu kuomba kura zetu, lakini hilo atalipitisha nani wakati wanaotunga sheria wengi wao ni walewale wenye ahadi za uongo kwetu?
Wagombea wengi wanajua hata wakiahidi kuwa mabomba yatatoa asali nchi nzima, waliopewa zawadi watakuwa wakishangilia bila kutafakari.
Inakuwaje mgombea akibanwa na wapiga kura anaeleza kuwa hawezi kutekeleza baadhi ya mambo aliyoahidi, aliwezaje kujinadi kwa ilani ya chama chake wakati huo mpaka hivi sasa ashindwe kutekeleza?
Zipo baadhi ya ahadi ambazo kwa kipindi hiki kilichobaki ni vigumu kuweza kutekelezeka na katika safu hii sitazitaja kwa sababu walioahidiwa wanakumbuka na walioahidi wanakumbuka zaidi.
Watanzania tunapaswa kujiuliza kwa nini tunadanganywa kirahisi na viongozi wetu halafu na sisi hatuoneshi kukasirishwa au kutoa adhabu pindi tunapogundua tumepewa ahadi hewa?Kama ahadi iliyotolewa na chama fulani ipo kwenye ilani yao (kwa maandishi) tunashindwaje kuidai? Nani atakayekuwa tayari kudai haki za wananchi kama wenyewe hawako mstari wa mbele kuzidai?
Kimsingi chama kinaposhindwa kutekeleza ilani yake tuna haki ya kukiuliza maswali mengi ili tujiridhishe na utendaji wake. Nia yangu ni kukumbusha tu kwamba wagombea wa vyama vyote katika nafasi ya urais, ubunge, udiwani na uwakilishi, wanakuja na ni vema kila mtu akajiandaa kuwauliza maswali.
Hakuna kitu kibaya kama kununuliwa . Tume ya Taifa ya Uchaguzi isiache mpiga kura anayestahili, kazi kwenu na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Damian Lubuva.

No comments:

Post a Comment