Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN
amewasili mjini Mbabane - Swaziland leo kwa ajili ya kuhudhuria mkutano
wa 36 wa Wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika- SADC-.
Makamu wa Rais SAMIA SULUHU HASSAN atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Muungano Tanzania Dakta JOHN MAGUFULI katika mkutano huo ambao
utafanyika tarehe 29 Agosti 2016 ambapo Tanzania inatarajiwa
kukabidhiwa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya hiyo.
Mkutano huo wa 36 wa SADC ni maalum kwa wakuu wa nchi na serikali
wanaounda Kamati ya siasa,ulinzi na usalama ambao watajadili kwa kina
hali ya siasa na usalama, demokrasia na maombi ya Burundi na Comoro kwa
ajili ya kujiunga na SADC.
Makamu wa Rais SAMIA SULUHU HASSAN katika msafara wake amefuatana na
Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Kikanda na
Kimataifa Augustine Mahiga, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji
Charles Mwijage na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar Amina Salum Ali.

