PART ONE: KUPATWA KWA JUA; DUNIA NA MWEZI TAREHE 1.09.2016; UKUTA wanasema nini? Serikali inazuia nini?
Tarehe 1.9.2016 ni siku iliyotangazwa ya maandamano nchi nzima.
Maandamano hayo yana jina la 'UKUTA' na yameandaliwa na Umoja wa Kupinga
Udikteta Tanzania.
Mpaka sasa ni Chadema pekee ndio wamejitokeza hadharani kama waasisi wa
'umoja' huo. Vyama vingine vya siasa viko kimya kuhusu 'tukio' hilo. Sio
tukio la kitaifa.
Ni vyema tujaribu kuangalia kilichoombwa na kilichozuiwa. Pia kuangalia sheria inasemaje kuhusu suala hili.
STAHILI (ENTITLEMENTS) ZA VYAMA VYA SIASA:
1. Sheria za Vyama vya Siasa (Political Parties Act) na za Jeshi la
Polisi (Police Force and Auxiliary Services Act) zinatoa stahili ya
kufanya mikutano ya hadhara (Public Meetings) na kuongozana
(Processions) kwa vyama vya Siasa kwa ajili ya kujitangaza na kutafuta
wanachama.
2. Pia sheria inatoa stahili ya kulindwa (Protection) na msaada
(Assistance) kutoka kwa vyombo vya usalama ili kufanikisha mikutano
kufanyika bila vurugu.
Kufanya mikutano ya hadhara na kuongozana Chama cha Siasa kinatakiwa
kutuma taarifa (Notification) masaa 48 kabla kwa Mkuu wa Polisi wa Eneo
(Police officer in charge of the area). Taarifa hiyo inatakiwa itaje
jina la chama, muda na eneo, sababu za mkutano kwa ujumla au jambo
lingine kama Waziri atakavyoelekeza.
Baada ya kutoa taarifa hiyo chama kinaruhusiwa kuendelea na mkutano au
kuongozana ISIPOKUWA tu kama kitapokea ZUIO (Stop Order) kutoka kwa
Polisi. Lazima Zuio liwe kwa maandishi na Polisi lazima itoe sababu ya
kuzuia.
Polisi haruhusiwi kutoa zuio isipokuwa tu i) kuna chama kingine kimeomba
kufanya mkutano au kuongozana au shughuli nyingine katika eneo hilo
hilo na muda uleule ii) mkutano huo unategemewa kutumika kwa sababu
ambazo ni kinyume na sheria, uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama wa
raia katika eneo hilo iii) kama chama hakijasajiliwa.... Hayo ndio
matakwa ya Sheria kwa ufupi.
End of Part One......
PART TWO: KUPATWA KWA JUA; DUNIA NA MWEZI TAREHE 1.09.2016; UKUTA wanasema nini? Serikali inazuia nini?
Tuanze na jina UKUTA; Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania. Je umoja huu
una 'uhalali' wa kisheria? Ni umoja unaotambulika na Sheria ya Vyama vya
Siasa? Je lengo lake ni kujitangaza au kupata wanachama wa chama cha
siasa? SIO HALALI KISHERIA.
Tuangalie neno MAANDAMANO (Demonstrations/Protests). Je mkutano wa
hadhara kujitangaza au kupata wanachama ni kitu kile kile na maandamano
ya kupinga Udikteta? Walichoomba Chadema kufanya tarehe moja ni nini kwa
mujibu wa Sheria? WANACHOOMBA SIO WANACHOTAKA KUFANYA.
Lakini pia tuangalie ZUIO LA RAISI: Raisi amepiga marufuku mikutano ya
kisiasa iwe ya hadhara au ya ndani. Polisi ndio wanaozuia. Je Raisi
anayo mamlaka kutoa zuio hilo? HANA MAMLAKA. Pia maagizo ya Raisi sio ya
kutolewa kwa mdomo!! Mwenye mamlaka ya kuzuia ni Polisi.
NINI KIFANYIKE?: Sheria inatoa nafasi kwa mtu ambaye amezuiwa na Polisi
(kwa Stop Order) kukata rufaa kwa Waziri husika. Uamuzi wa Waziri ni wa
mwisho. Kukata rufaa hakutakuwa na matokeo tofauti. Waziri hawezi kwenda
kinyume na Raisi wake. HAIWEZEKANI.
Je, Mahakama inahitaji kutoa tafsiri? Sidhani kama kuna kisichoeleweka
kwa pande zote mbili. Kuna uwezekano wa 'maamuzi ya pamoja' ya
kutokuelewa. Mahakama itatumika aidha kubariki kutokuelewa kwa upande
mmoja wapo au kulichanganya suala hili la kisiasa na sheria.
Chadema wanatakiwa kuachana na 'maandamano'. Jina walilochagua na "nia
yao njema" haviendani! Wasitegemee huruma ya wananchi. Kulazimisha UKUTA
kuendelea ni kukaribisha mvurugano kati ya polisi na wafuasi wao. Hiyo
itakuwa ni tafsiri ya uvunjifu wa amani ambayo polisi watatumia!! Na
uvunjifu wa amani ni kichaka kikubwa sana kujificha!
Serikali itafakari upya. Raisi asikilize ushauri. Yeye atekeleze ahadi
na aachane na siasa za wapinzani. Hana sababu ya kuogopa vivuli. Yeye na
chama chake wana deni la maendeleo kwa wananchi. Makatazo yake ndio
chanzo cha 'maandamano' ya kumpinga. Kukataa kuwasikiliza wapinzani na
kuendelea kuamini kwamba yuko SAHIHI kwa sababu ni Raisi anakosea. Hili
ni tatizo la KUJITOA UFAHAMU Raisi; Chadema na Polisi Wanajua.
PART THREE: KUPATWA KWA JUA; DUNIA NA MWEZI TAREHE 1.09.2016; UKUTA wanasema nini? Serikali inazuia nini?
Hili ni tatizo la KUJITOA UFAHAMU Raisi, Chadema na Polisi. Wote wanajua
na wanaelewa sheria inasemaje, wana stahili/haki zipi na kwa utaratibu
gani!
Ushauri wangu wananchi wakae majumbani. Hao watatu wakutane barabarani
katika kupatwa kwao. Tutatoa pole na kuchangia damu. Kwenye giza
tutabaki.