![]() |
Vikao hivyo vinapangwa kufanyika wakati mkutano wa nne ukianza rasmi kesho, baada ya kuahirishwa mwishoni mwa Juni mwaka huu wakati wa mkutano wa Bajeti.
Mbunge wa Vunjo (NCCR- Mageuzi), James
Mbatia alieleza jana kuwa uamuzi wa kufanya vikao hivyo umefikiwa baada
ya upinzani kukaa kikao na viongozi wa dini Agosti 24 mwaka huu ili
kutafuta suluhu ya kudumu.
“Kikao cha kwanza tutakaa kamati ya
uongozi ya wabunge wa upinzani kujadili suala hilo na baadaye
tutamaliza na kikao cha wabunge wote ili kubaini njia endelevu za
kumaliza jambo hilo,” alisema Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Wabunge wa Ukawa wamekuwa wakisusia
vikao vinavyoendeshwa na Naibu Spika kwa madai ya kutoridhishwa na
uongozi wake tangu Mei mwaka huu, baada ya Dk Tulia kukataa kujadili
hoja ya kufukuzwa wanafunzi zaidi ya 8,000 stashahada ya ualimu wa Chuo
Kikuu cha Dodoma (Udom).
Hata wakati wakisubiri kufanyika vikao
hivyo ambavyo Mbatia hakutaka kuelezea kwa undani, upinzani ulitangaza
kurudi bungeni baada ya mkutano wao na viongozi wa dini.
Katika mkutano na wanahabari Agosti
25, Mbatia kwa niaba ya vyama vilivyoshiriki mkutano huo wakiwamo
ACT-Wazalendo, alisema wangejadiliana namna ya kufanikisha jambo hilo
kama sehemu ya kutii ushauri wa viongozi hao wa kiroho.
Hata hivyo, haijawekwa bayana iwapo kesho Ukawa wataendelea na vikao hata kama Dk Tulia ataendelea kuongoza kiti hicho ama la.
Mbatia alisema jana kuwa watatoa taarifa rasmi leo namna vikao hivyo vitakavyofanyika na siku husika.
Mbatia alisema jana kuwa watatoa taarifa rasmi leo namna vikao hivyo vitakavyofanyika na siku husika.
Kuhusu kupata taarifa ya mwenendo wa
mchakato wa kutafuta maridhiano ulioelezwa na Spika Job Ndugai hivi
karibuni, Mbatia alisema hawajapata chochote na wao wanasikia kwenye
vyombo vya habari kama wengine.
Alipoulizwa ni lini vikao vya
maridhiano kati ya pande hizo yataanza, Ofisa Habari, Elimu na
Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya alisema Spika anatarajiwa kufika
ofisini leo na kwamba kama ataona kuna haja ya kufanya hivyo atapanga
utaratibu wa namna anavyoona inafaa.
