WAKAZI wawili wa Kijiji cha Bukigi kilichopo Kata ya Malampaka mkoani
Simiyu, wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kupatikana na viungo vya
binadamu.
Waliofikishwa juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Maswa mbele wa Hakimu
Tumaini Marwa, ni Matheyo Yumbu (50) na Juma Mihangwa (28).
Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Nassibu Swedy
kuwa Mei 5, mwaka huu, saa 11 alfajiri katika Kijiji cha Bukigi,
washitakiwa hao walikutwa wakiwa na viungo hivyo.
Alidai viungo walivyokutwa navyo washitakiwa hao ni fuvu la kichwa,
mifupa ya miguu na mikono ya binadamu wakiwa wamevihifadhi katika mfuko
wa sandarusi katika nyumba waliyoishi.
Hata hivyo, washtakiwa hao walikana kosa hilo na kunyimwa dhamana na
walipelekwa mahabusu hadi hapo kesi itakapotajwa tena Mei 29, mwaka huu
na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

No comments:
Post a Comment