SAA chache baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kukipiga
Yanga akitoka Mgambo JKT, kiungo mshambuliaji Malimi Busungu amefichua
kilichomfanya asaini fomu za Jangwani.
Hakuna aliyekuwa akitarajia kama mchezaji huyo
angemwaga wino Jangwani wakati ilikuwa ikielezwa kuwa viongozi wa Simba
walikuwa wakizunguka naye kwenye magari ili kumshawishi ajiunge na timu
yao.
Akizungumza na Mwanaspoti muda mchache baada ya
kusaini Yanga, Busungu alifichua siri ambayo hakuna aliyekuwa akiijua
dhidi yake.
Busungu alisema sakata la winga teleza wa Simba,
Ramadhani Singano ‘Messi’ dhidi ya viongozi wake, ndilo lililomfanya
aamue kuitosa Simba.
“Unajua mimi ni kijana mdogo, pia soka ndiyo
maisha yangu, hivyo nilipokuwa nasikiliza mzozo wa Messi na viongozi wa
Simba, nikabaini kuwa Msimbazi kuna ubabaishaji mkubwa,” alisema.
“Hata wakati nikifanya mzungumzo na viongozi wa
klabu hiyo, nilibaini wengi ni wajanja wajanja na kuhisi
linalolalamikiwa na Messi ndiyo utaratibu wa klabu hiyo na kuamua
kuwatosa,” alisema.
Busungu alisema anaamini kutua kwake Yanga
kutakuwa msaada mkubwa katika mustakabali wa maisha yake ya soka, hasa
akitambua kuwa ni klabu itakayoshiriki michuano ya kimataifa mwakani
(Ligi ya Mabingwa Afrika), hivyo kuwa na nafasi ya kujitangaza katika
anga hizo.
“Michuano ya CAF na umakini wa viongozi wa Yanga
hata wakati nazungumza nao, ni uthibitisho kuwa inaongozwa na watu
makini na wenye malengo, tofauti na Simba, ingawa siwezi kuibeza,”
alisema.
No comments:
Post a Comment