Serikali ya Burundi imekariri kuwa
rais Pierre Nkurunziza hatajiondoa kutoka kinyanganyiro cha urais licha
ya nchi hiyo kukabiliwa na wimbi la maandamano.
Awali vyama vya upinzani vilikuwa vimepinga ratiba mpya ya uchaguzi iliyotolewa na tume huru ya uchaguzi nchini humo wakihoji uhalali wa ratiba hiyo inayotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha majuma mawili yajayo.Wakati huohuo, afisa mmoja wa ngazi ya juu katika umoja wa mataifa ameonya kuwa kundi la wanamgambo wanaounga mkono serikali wamekuwa wakiendeleza ukatili dhidi ya wale wanaopinga uamuzi wa rais Nkurunziza kuwania awamu ya tatu madarakani.
Kamishna huyo wa kitengo cha umoja wa mataifa kinachohusika na haki za kibinadamu, Zeid Ra'ad Al Hussein amesema wanamgambo hao wanaoiuunga mkono serikali wametuhumiwa kuhusika katika vitendo vya mauji , kuwapiga na kuwanyanyasa baadhi ya wapinzani na kuitaka serikali kukemea na kukomesha vitendo hivyo.
Kitengo hicho cha umoja wa mataifa chasema kimekuwa kikipokea simu kutoka pande mbalimbali za Burundi kulalamikia vitendo kama hivyo na hasa kutishwa na wanaosemekana kuwa wafuasi wa kundi hilo linalojiita Imbone-rakure.
No comments:
Post a Comment