ARSENE Wenger kiboko yao. Mfaransa huyo ameweka rekodi ya kuwa
kocha wa kwanza kubeba ubingwa wa Kombe la FA mara sita tangu
ilipokwisha Vita ya Pili ya Dunia.

Jumamosi Wenger aliishuhudia Arsenal yake ikiichapa Aston Villa mabao 4-0 na kubeba taji hilo, rekodi inayomfanya amfikie George Ramsey, ambaye mara ya mwisho alibeba taji hilo akiwa na Aston Villa mwaka 1920.
Mabao ya Theo Walcott, Alexis Sanchez, Per
Mertesacker na Olivier Giroud yalitosha kwa Arsenal kutetea ubingwa huo
wa Kombe la FA tena kwa ushindi wa mabao mengi kwenye fainali kwa mara
ya kwanza tangu mwaka 1994.
Ushindi huo umeandika historia pia kwa Arsenal kwa
kubeba taji hilo lenye hadhi kubwa Uingereza kwa mara ya 12 na kuwapiku
Manchester United katika historia ya kimafanikio ya michuano hiyo.
“Najivunia,” alisema Wenger.
“Kama haijawahi kufanywa basi inaonyesha jinsi
ilivyokuwa ngumu. Kila mtu anapenda kufanikiwa katika vitu vigumu.
Binafsi nimecheza fainali saba za Kombe la FA na nimeshinda sita,
najivunia jambo hilo. Ni jambo zuri kwa klabu pia kwa sababu hili ni
taji la 12 la ubingwa wa FA.”
Baada ya kushinda fainali iliyopita kwa ushindi wa
dakika za nyongeza dhidi ya Hull City msimu uliopita, Wenger amefurahi
kwa namna kikosi chake kilivyomaliza kazi mapema kwenye fainali hiyo ya
juzi na kushinda kwa kishindo.
Kocha Mkuu wa Aston Villa, Tim Sherwood, amekubali
kuhusu kiwango cha Arsenal kilichoonyeshwa kwenye fainali hiyo na
kukiri kwamba wakali hao wa Emirates walistahili kushinda.
“Wamestahili kushinda, hakuna mjadala juu ya hilo.
Walikuwa kwenye ubora mkubwa na wanasoka wao wa viwango vya dunia
wamefanya mambo makubwa uwanjani,” alisema Sherwood.
“Siwezi kutoa kisingizio. Kwa kusema ukweli zile
bao 3-0 zilikuwa zinatosha kwa sababu ni kama zimekufanya kuwa mgonjwa
na unahitaji kumeza dawa, lakini wakafunga jingine la nne ambalo mimi
nililiona kama teke la sehemu za siri.
“Nimekuwa mgonjwa na nadhani hata wachezaji
watakuwa hivyo pia. Lilikuwa somo tosha kwetu. Tunahitaji kujenga timu
mpya, wachezaji wanapaswa kufahamu namna ya kuwa washindi.”
Baada ya ushindi huo, Wenger anaamini kikosi chake
sasa kinapaswa kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ujao na
amewataka wachezaji wake kufanikisha hilo jambo ambalo limeungwa mkono
pia na fowadi Theo Walcot.
No comments:
Post a Comment