STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe, amemshauri straika mwenzake,
Laudit Mavugo, kuwa atakapotua Simba ajitume zaidi huku pia akisisitiza
ni mchezaji ambaye anaweza kusaidia Simba kwa kiasi kikubwa.
|
Mavugo alifuatwa Burundi na Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Simba na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Collin Frisch
ambaye ilidaiwa kuwa angemsainisha mkataba huo baada ya kukwama kuja
nchini wiki iliyopita kutokana na majukumu ya kikosi chake cha timu ya
Taifa.
Tambwe ambaye msimu uliopita aliichezea Simba na
kuachwa katika usajili wa dirisha dogo, aliliambia Mwanaspoti kuwa
kiwango cha Mavugo ni kizuri ili mradi apate ushirikiano wa kutosha
kutoka kwa wachezaji na viongozi wa Simba.
“Simba ni timu nzuri sana ina wanachama na
mashabiki wazuri, ila tatizo lipo kwa viongozi ambao wengi wanaonekana
kuwa wababaishaji na kama wataendelea na ubabaishaji wao hawatafika
popote, naamini Mavugo atawasaidia sana kwani ni mchezaji mzuri na
anajitambua,” alisema Tambwe.
Tambwe aliweka wazi kwamba kabla ya Mavugo kufikia makubaliano na viongozi wa Simba alimuuliza juu ya mfumo wa soka la Tanzania.
“Aliniuliza alipopigiwa simu tu, nilimwambia
ukweli kwamba soka la Tanzania ni zuri ila lina changamoto kubwa kutoka
kwa viongozi wa klabu anayokwenda,” alisema.
“Namfahamu Mavugo alipokuwa akicheza hapa na
baadaye kwenda Rwanda, ndio maana alipopigiwa simu aliniuliza mambo
mbalimbali kuhusiana na Tanzania, ni kweli angekuja huko ila kocha wetu
wa timu ya Taifa alimwambia wazi kwamba angeamua kuja Tanzania
kumalizana na Simba na kuacha timu ya Taifa basi huo ungekuwa ndiyo
mwisho wake wa kuichezea timu hii, ndio maana hakuja.
“Kikubwa nilichomshauri ni kujituma na kufanya
kazi iliyompeleka akisikiliza maneno basi anaweza kuvurugikiwa na
asifanye vizuri.
“Nilimtaka ajitambue na kuongeza juhudi zaidi
maana mashabiki wa Tanzania ukiharibu kidogo nao hawachelewi kukugeuzia,
ila Simba ni timu nzuri tatizo ni viongozi.”
Simba inamsajili Mavugo ambaye ni raia wa Burundi
akitokea Vital’O ya Burundi ingawa kabla ya kutua katika timu hiyo
aliwahi kuzichezea Kiyovu na Polisi za Rwanda.
Mavugo mwenye mabao 32 msimu huu, anakuwa mchezaji
wa tano wa kigeni wa Simba baada ya Emmanuel Okwi, Juuko Murshid,
Raphael Kiongera na Simon Sserunkuma.
No comments:
Post a Comment